هود
هذه ترجمة لتفسير السعدي كما ينشرها IslamHouse.com في saadi.islamenc.com، مقروءةً من صفحات ذلك الموقع. لا يذكر الموقع من ترجمها ولا أي طبعة مطبوعة تتبعها، ولا يذكر شروطًا لأخذ نصّها، ولذلك لم يُتحقق من حق عرضها. لم يقارنها أحد بكتاب مطبوع، ولم يراجعها أحد من العلماء. يقف كل مقطع بجانب الآيات التي يعلّق عليها، وهي نص القرآن من Tanzil كما هو عنده؛ والآية التي لا يعطيها الموقع شرحًا خاصًّا بها تقف مع المقطع الذي قبلها، ويسمّي الفهرس كل آية من هذا النوع. لم يكتب سبيل شيئًا منها ولم يترجمه.
النص منsaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)أُخذ في 2026-10-22
كَأَن لَّمْ يَغْنَوْا۟ فِيهَآ ۗ أَلَا بُعْدًا لِّمَدْيَنَ كَمَا بَعِدَتْ ثَمُودُ ٩٥
{95} "Kama kwamba hawakuishi kwa ustawi humo." Yaani, ni kana kwamba hawakukaa katika makazo yao wala hawakufurahia humo wakati adhabu ilipowajia. "Zingatia ilivyoangamia Madyana," wakati Mwenyezi Mungu alipoiangamiza na kuihizi, "kama ilivyoangamia Thamud." Yaani, makabila haya mawili yalishiriki katika kufutiliwa mbali na kuangamia. Naye Shu'aib - amani iwe juu yake - alikuwa akiitwa mhubiri wa manabii, kwa sababu ya kuwashawishi kwake kaumu yake kwa uzuri. Na kuna faida na mafunzo mengi katika kisa chake: Miongoni mwake ni kwamba, makafiri namna watakavyoadhibiwa juu ya kuacha msingi wa Uislamu, basi vile vile wataadhibiwa kwa kuacha sheria zake na matawi yake. Kwa sababu, Shu'aib aliwalingania kaumu yake kwenye tauhidi na kutimiza vipimo na mizani, na akatoa ahadi ya adhabu juu ya kuacha jumla ya hayo. Miongoni mwake ni kwamba, kupunguza vipimo na mizani ni katika madhambi makubwa na anahofiwa adhabu ya haraka mwenye kufanya hivyo, na kwamba hayo ni katika kuiba mali za watu. Na ikiwa wizi wao katika vipimo na mizani unasababisha ahadi ya adhabu, basi kuiba kwao kwa njia ya nguvu na ushindi ni jambo wanalostahiki na kufailia zaidi kuadhibiwa. Miongoni mwake ni kwamba malipo ni ya aina sawa na matendo. Kwa hivyo, mwenye kupunja mali za watu akitaka kuongeza mali yake, basi anaadhibiwa kwa kinyume cha hilo, na linakuwa ndiyo sababu ya kutoweka kwa heri ya riziki aliyokuwa nayo. Kwa kauli yake "hakika mimi ninawaona mmo katika hali njema." Yaani, kwa hivyo msisababishe kutoweka kwake kwa matendo yenu. Miongoni mwake ni kwamba, ni lazima kwa mja aridhike na yale aliyopewa na Mwenyezi Mungu na aridhike na yale ya halali juu ya yale yaliyoharamishwa, na machumo yanayoruhusiwa juu ya yale yaliyoharamishwa, na kwamba hayo ni bora kwake. Kwa sababu ya kauli yake, "Alivyowabakishia Mwenyezi Mungu ndiyo bora kwenu" kwa maana katika hayo kuna baraka nyingi na kuongezeka kwa riziki katika hilo ambazo haziko katika kupigania mambo yaliyoharamishwa kama vile kuondolewa baraka na ni kinyume cha baraka. Miongoni mwake ni kwamba, hilo ni katika yale yanayofungamana na imani na athari zake, kwa maana alifungamanisha kuyafanya juu ya kuwepo imani, kwa hivyo likaashiria kwamba ikiwa mateso hayapo, basi Imani ni pungufu au haipo kabisa. Miongoni mwake ni kwamba, Swala haikuacha kuwa ni ibada inayoruhisiwa kwa Mitume wa zamani, na kwamba ni miongoni mwa matendo bora zaidi, kiasi kwamba ubora wake umethibiti kwa makafiri na kupewa kwake kipaumbele kuliko matendo mengine yote, na kwamba inakataza uchafu na uovu, nayo ndiyo mizani ya imani na sheria zake. Kwa hivyo kwa kuisimamisha, hali za mja zinakamilika, na kwa kutoisimamisha, hali zake za kidini yanakuwa na kasoro. Miongoni mwake ni kwamba, mali ambayo Mwenyezi Mungu humruzuku mtu, hata kama Mwenyezi Mungu amempa, basi hana haki ya kufanya humo chochote anachotaka. Kwani, ni amana kwake, na ni lazima aisimamishe haki ya Mwenyezi Mungu kwa kutekeleza haki zilizoko ndani yake na kujiepusha na mapato ambayo Mwenyezi Mungu na Mtume wake wameharamisha, si kama wanavyodai makafiri na mwenye kufanana nao, kwamba mali zao wanaweza kufanya humo chochote wanachotaka na kuchagua, sawa iafikiane na hukumu ya Mwenyezi Mungu au ihalifiane nayo. Miongoni mwake ni kwamba, katika kinachokamilisha ulinganizi wa mlinganiaji na kukitimiza ni kwamba awe wa kwanza kuyafanya yale anayoamrisha wengine wayafanye na wa kwanza kuacha yale ambayo anawakataza wengine. Kama alivyosema Shu'aib, amani iwe juu yake: "Wala mimi sitaki niwahalifu nikafanya yale ninayowakataza." Na kwa kauli yake Mtukufu "Enyi mlioamini! Kwa nini mnasema msiyoyatenda? [Yanachukiza vikubwa mno kwa Mwenyezi Mungu kuwa mnasema msiyoyatenda]." Miongoni mwake ni kwamba kazi ya Mitume, na desturi yao, na mila yao ni kutafuta kurekebisha kulingana na uwezo na uwezekano, ili wafikie kuleta masilahi na kuyakamilisha au kuleta kile kinachoweza kufikiwa katika hayo, na kuzuia maovu na kuyapunguza, na wanayazingatia masilahi ya umma kuliko masilahi kibinafsi. Na uhakika wa masilahi ni yale ambayo kwayo hali za waja zinatengenea, na mambo yao ya kidini na ya kidunia yananyooka kwayo. Miongoni mwake ni kwamba, mwenye kufanya analoweza kufanya la kutengeneza, basi hatalaumiwa wala kushutumiwa katika kutofanya kwake asichoweza kufanya. Kwa hivyo, ni juu ya mja kusimamisha mambo ya kutengeneza katika nafsi yake na kwa wengine kulingana na awezavyo. Miongoni mwake ni kwamba, mja hafai kuitegemea nafsi yake kiasi cha kupepesa jicho, bali asiache kuendelea kuomba msaada kutoka kwa Mola wake Mlezi, na kumtegemea Yeye, na kumwomba mafanikio. Na anapofikiwa na kitu katika mafanikio, basi na akinasibishe na bwana wake na yule aliyekileta, wala asijinasibishie yeye mwenyewe. Kwa mujibu wa kauli yake: "Na sipati kuwezeshwa haya isipokuwa na Mwenyezi Mungu. Kwake Yeye ninategemea, na kwake Yeye ninarudi." Miongoni mwake ni vitisho kwa maangamivu ya umma mbalimbali, na yale yaliyowapata, na kwamba inapasa kutaja visa ambavyo ndani yake kuna kuwaadhibu wahalifu katika muktadha wa mawaidha na makaripio. Na vile inapasa kutaja kile ambacho Mwenyezi Mungu aliwakirimia kwacho watu wachamungu wakati wa kutia moyo na kuhimiza juu ya uchamungu. Miongoni mwake ni kwamba, mwenye kutubia dhambi kama vile anavyosamehewa dhambi yake na kuachiliwa, basi Mwenyezi Mungu Mtukufu anampenda na anamuenzi sana, na wala hayaangaliwi maneno ya wale wanaosema: hakika mwenye kutubia anapotubu, basi inamtosha tu kusamehewa na kuachiliwa. Na ama kumuenzi na kumpenda, basi hilo halipati. Lakini ukweli si hivyo, kwa maana Mwenyezi Mungu alisema, "Na ombeni msamaha kwa Mola wenu Mlezi, tena tubuni kwake. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kurehemu sana, Mwenye upendo mkubwa." Miongoni mwake ni kwamba, Mwenyezi Mungu huwalinda Waumini kwa sababu nyingi, baadhi yake wanaweza zijua na hata pengine wanaweza kosa kujua chochote katika hizo. Na pengine akawalinda kwa sababu ya kabila lao na makafiri wa nchi yao, kama Mwenyezi Mungu alivyomlinda Shu'aib kutokana na kupigwa mawe na kaumu yake kwa sababu ya kundi lake. Na kwamba, hakuna ubaya wowote katika kujitahidi katika mafungamano haya ambayo kwayo mtu anaweza kuulinda Uislamu na Waislamu, bali pengine hilo likawa lazima. Kwa sababu kutengeneza kunahitajika kulingana na uwezo na uwezekano. Kwa hivyo, lau kuwa Waislamu watawasaidia wale walio chini ya uongozi wa makafiri, na wakajitahidi kuufanya uongozi huo kuwa jamhuri ambayo watu binafsi na makabila wataweza kutekeleza haki zao za kidini na za kidunia, basi ingelikuwa bora kwao kuliko kujisalimisha kwa nchi ambayo inaondoa haki zao za kidini na za kidunia, na wanawania kuwaangamiza na kuwafanya watenda kazi na watumishi wao. Ndiyo, ikiwezekana nchi hiyo iwe ya Waislamu na wao ndio watawala, basi hilo ndilo la lazima kufanywa. Lakini kwa sababu cheo kutowezekana kwa daraja hii, basi daraja ambayo ndani yake kuna kuizuia na kuilinda dini na dunia itatangulizwa. Na mwenyezi Mungu ndiye anayejua zaidi.