يونس
هذه ترجمة لتفسير السعدي كما ينشرها IslamHouse.com في saadi.islamenc.com، مقروءةً من صفحات ذلك الموقع. لا يذكر الموقع من ترجمها ولا أي طبعة مطبوعة تتبعها، ولا يذكر شروطًا لأخذ نصّها، ولذلك لم يُتحقق من حق عرضها. لم يقارنها أحد بكتاب مطبوع، ولم يراجعها أحد من العلماء. يقف كل مقطع بجانب الآيات التي يعلّق عليها، وهي نص القرآن من Tanzil كما هو عنده؛ والآية التي لا يعطيها الموقع شرحًا خاصًّا بها تقف مع المقطع الذي قبلها، ويسمّي الفهرس كل آية من هذا النوع. لم يكتب سبيل شيئًا منها ولم يترجمه.
النص منsaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)أُخذ في 2026-10-22
إِنَّ ٱلَّذِينَ لَا يَرْجُونَ لِقَآءَنَا وَرَضُوا۟ بِٱلْحَيَوٰةِ ٱلدُّنْيَا وَٱطْمَأَنُّوا۟ بِهَا وَٱلَّذِينَ هُمْ عَنْ ءَايَـٰتِنَا غَـٰفِلُونَ ٧
{7} Yeye Mtukufu Anasema, "Hakika wale wasiotaraji kukutana nasi;” yaani, hawataki kukutana na Mwenyezi Mungu ambaye ndiye mkubwa zaidi ambaye watamanio wanatamani, na wa juu zaidi anayetumainiwa na wanaotumaini. Lakini wao walilipa mgongo, na hata huenda walilikadhibisha “na wakaridhia uhai wa dunia hii” badala ya Akhera, "na wakatua nao.” Yaani, waliyategemea, na wakayafanya kuwa ndio lengo la jambo lao na mwisho wa makusudio yao. Basi wakayatafuta kwa bidii, na wakashikana na starehe zake na matamanio yake, na wakazitafuta kwa njia yoyote ile ziwezavyo kupatikana, na kwa upande wowote ule zinapoonekania, wanaziendea haraka. Walielekeza matashi yao, na nia zao, na fikira zao, na matendo yao kwazo. Basi ni kana kwamba waliumbwa kubaki humo, na ni kana kwamba si nyumba ya kupitia tu ndani yake, ambayo wasafiri wanachukua humo masurufu kwa ajili ya nyumba ya milele ambayo humo ndiko wataenda wa mwanzo na wa mwisho, na ambayo kwa ajili ya neema zake na starehe walijiandaa wale waliofanikishwa "na wale walioghafilika na Ishara zetu.” Kwa hivyo hawafaidiki na ishara za kiqur-aani wala ishara za kiupeo na kinafsi. Na kuupa ushahidi mgongo kunalazimu kukipa mgongo na kughafilika na kile kinachoashiriwa, na kinachokusudiwa.